Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Shab Zendehdar, Katibu wa Baraza Kuu la Hawza, mwanzoni mwa somo lake la juu la Fiqhi lililofanyika katika Msikiti Mkuu (Masjid A‘zam) mjini Qum Iran, alizungumzia hatua ya serikali ya Jamhuri ya Azerbaijan ya kuwapiga marufuku wasichana wanaovaa hijabu kuhudhuria shule pamoja na hatua ya kuwalazimisha wanawake kuvua hijabu zao.
Akizungumzia suala hilo, alisema: “Tunatumaini kwamba viongozi wa serikali ya Azerbaijan wataamka na kuacha dhuluma hii kubwa wanayoifanya dhidi ya wanawake wanaovaa hijabu nchini humo.”
Aliongeza kuwa baadhi ya nchi za Kiislamu zimeiga makafiri na wapinzani wa Uislamu, na zimezuia uvaaji wa hijabu hata kwa wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi na sekondari.
Kwa kweli, inasikitisha sana kuona jinsi hukumu za Mwenyezi Mungu zinavyokanyagwa, ilhali suala la hijabu ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu. Vilevile, watu wanaotaka kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu wananyimwa haki ya kupata elimu.
Katibu wa Baraza Kuu la Hawza alieleza kwamba; uzoefu umetuthibitishia kuwa kutovaa hijabu na kuenea kwa utupu katika jamii huharibu na kupotosha jamii pamoja na vijana, na pia huzuia maendeleo na ustawi wao.
Ayatullah Shab Zendehdar aliendelea kusema kwamba; nchi ambazo hazikuyapa umuhimu masuala haya kwa sasa zimejikuta katika hali mbaya na matatizo makubwa. Kisha akasoma Aya ya 124 ya Suratu Twaha, ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنْكًا
“Na atakayejiepusha na ukumbusho Wangu, basi kwa hakika atakuwa na maisha yenye dhiki.”
(Twaha: 124).
Alimalizia kwa kusema: “Tunatumaini kwamba viongozi wa serikali ya Azerbaijan nao wataamka na kuacha dhuluma hii kubwa wanayoifanya dhidi ya wanawake wanaovaa hijabu nchini humo.”
Maoni yako